Mwanasheria Mkuu aunga mkono hoja ya Mh. Pinda

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema inaunga mkono pendekezo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwataka wanasheria wa pande mbili za Muungano wakutane ili kutoa tafsiri sahihi juu ya `nchi na taifa`.
 
Hayo yalielezwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Bw. Idd Pandu Hassan kufuatia mvutano uliojitokeza juu ya Zanzibar ni nchi au si nchi. 
Bw. Pandu alisema msimamo wa SMZ uko `palepale` kwamba unatambua kuwa Zanzibar ni nchi kulingana na Katiba ya Zanzibar inavyoeleza.
 
``Mimi binafsi naunga mkono uamuzi wa Waziri Mkuu kututaka wanasheria wakuu kukutana kupitia Katiba na kutafuta ufumbuzi katika maeneo yenye kasoro 
kwa vile ndio kazi yetu,`` alisema Mwanasheri Mkuu.
 
Alisema baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Zanzibar ilifuta utaifa wake kama ilivyofuta Tanganyika na kuundwa taifa la Tanzania.
 
Alieleza kimsingi si taifa, lakini ni nchi na ndio maana ina mamlaka kamili, ikiwemo Utawala, Baraza la Wawakilishi na Mahakama.
 
Bw. Pandu ambaye ni mwanasheria mkongwe Zanzibar, alisema baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kiti cha Zanzibar katika Umoja wa Mataifa kilifutwa na kubakia kiti kimoja cha Tanzania.
 
Hata hivyo, alisema serikali ya Tanganyika iliingizwa ndani ya Serikali ya Muungano, lakini Serikali ya Zanzibar iliendelea kubakia.
 
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo Bungeni juzi, alisema eneo la ardhi Tanzania Bara na katika visiwa vya Zanzibar lote ni la Jamhuri ya Muungano pamoja na eneo la usawa wa bahari ya Hindi.
 
Alisema kimsingi Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza wazi kuwa Tanzania ni nchi moja, yenye serikali mbili ikiwemo ya Muungano na Zanzibar.
 
``Ninasikia suala hili limeleta msuguano huko kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar, lakini Katiba iko wazi kuwa kuna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ni sheria mama inayotuongoza wote na ile ya Zanzibar ambayo katika kipengele kimoja inasema kuwa Zanzibar ni nchi, lakini inapotokea mgongano kama huo sheria mama iliyo juu ni ile ya Muungano,`` alisema Waziri Mkuu Pinda.
 
Hata hivyo, alisema pamoja na kuwa suala hilo liko wazi ni vyema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano na yule wa Zanzibar wakakaa na kuchambua ili watoe tafasiri sahihi.
 
Wakichangia bajeti ya Wizara ya Nchi, ofisi ya Rais, Katiba na Utawala Bora, wajumbe saba wa Baraza la Wawakilishi waliitaka SMZ itoe tamko juu ya kauli ya Waziri Mkuu kuwa Zanzibar ni nchi au si nchi.
 
`Kauli niliyoitoa iko pale pale sina jambo lingine jipya, lakini naafiki hatua aliyoichukua Waziri Mkuu kututaka tukutane ni muafaka,`` alisema Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.